KIBABII UNIVERSITY 

Mhadhara wa Kwanza wa Umma Kumuenzi Ken Walibora

Katika hafla ya kipekee, wanafunzi, wahadhiri, na wafanyikazi wa Chuo Kikuu cha Kibabii, pamoja na wageni waalikwa na umma kwa jumla, walijumuika Chuoni humo kumuenzi msomi, mwandishi na mwanahabari tajika, Ken Walibora, mnamo tarehe 9 Aprili, 2024.

Mgeni Rasmi, Prof. F.E.M.K. Senkoro alikaribishwa chuoni Kibabii na kupokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Isaac Ipara Odeo, kwa ajili ya hafla hio. Kabla ya hafla kuanza rasmi pale ukumbini C, wageni walielekezwa ugani katika kona lililotengewa shughuli ya upanzi wa miti kumkumbuka hayati. Upanzi huo wa miti ulishuhudiwa na wageni wa heshima walioalikwa, wakiwemo Makamu Mkuu wa Chuo cha Kisii, Prof. Nathan Ogechi, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Africa Mashariki, Prof. Inyani Simala, na viongozi wa ngazi ya juu chuoni wakiwemo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala, Fedha na Maendeleo, Prof. Donald Siamba, Kaimu Naibu Makamu wa Chuo, Taaluma na Maswala ya Wanafunzi, Prof. Stanley Mutsotso, na mwakilishi wa Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Ushirikiano, Utafiti na Ubunifu, Prof. Samwel Mbugua. Wengine walioshuhudia shughuli hio ya upanzi wa miti ni Msajili wa Maswala ya Kitaaluma, Sr. Dr. Jacklyne Alari, Mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Utamaduni (KITALU), Prof. Ernest Mohochi, mwanachama wa Bodi ya KITALU, Dkt. Felix Orina, mwenyekiti wa CHAKITA, Dkt. Fred Simiyu, na mwenyekiti wa kamati andalizi ya mhadhara huo wa kwanza wa umma, Dkt. Henry Nandelenga.

Nduguye mkubwa Ken Walibora, Bw. Patrick Lumumba, alisafiri kutoka Cherangany kuwakilisha Jamii ya Ken Walibora na kujiunga na udugu wa Chuo Kikuu cha Kibabii kumuenzi hayati. Alisema kwamba Ken Walibora aliguza maisha ya wengi kutokana na matendo yake mema, maandishi yake, na safari yake ya Kiswahili. Alishukuru Chuo Kikuu cha Kibabii kwa kuandaa hafla ya aina yake ya kumkumbuka Ken Walibora.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Kisii, Prof. Nathan Ogechi alieleza furaha yake kuwa Chuoni Kibabii kwa shughuli hio muhimu na kumshukuru Prof. Ipara Odeo, ambaye alikuwa mwalimu wake, kwa kuandaa hafla hio ya kipekee ya kumuenzi Ken Walibora. Prof. Ogechi alieleza waliohudhuria kuhusu safari yake ya Kiswahili ambayo ilikuwa na changamoto mingi na jinsi ambavyo safari ya Kiswahili ya Ken Walibora ilivyomtia moyo na kumuwezesha kufanikiwa katika safari yake hadi akawa Professa wa Kiswahili.

Prof. Ipara Odeo alimtambulisha Mgeni Rasmi kama mtu mcheshi aliyeelewa vizuri falsafa na safari ya Kiswahili ya Ken Walibora. Prof. Ipara alieleza wahudhuriaji kwamba Prof. Senkoro alizaliwa Pare, Kilimanjaro, na safari yake ya Kitaaluma ilianza alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnamo mwaka 1972. Prof. Senkoro aliendeleza masomo yake hadi alipotunukiwa shahada ya uzamifu katika Kiswahili. Bidii yake ilimfanya akakwea ngazi za kitaaluma kwa haraka hadi akawa Professa tajika wa Kiswahili. Prof. Senkoro amefunza katika vyuo vikuu vingi duniani vikiwemo Dar es Salaam, Harvard na Princeton alipojenga ukuruba na Ken Walibora. Prof. Ipara alitambua juhudi za Prof. Senkoro katika safari  ya Kiswahili ya Ken Walibora. Alimalizia wasilisho lake kwa kusema kuwa Chuo Kikuu cha Kibabii kimetoa heshima kubwa kwa Ken Walibora kwa kuanzisha Kitengo cha Mikusanyo za kazi zake katika Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Kibabii.

Katika hotuba yake, Prof. Senkoro aliwakumbusha wahudhuriaji ya kwamba wamekusanyika kusherehekea maisha ya Ken Walibora na kazi zake, wala sio kulia na kusikitika. Alieleza safari ya Kiswahili ya Ken Walibora kuanzia masomo yake, kazi yake ya ualimu, uandishi, na kazi yake ya uanahabari. Alimtambua Ken Walibora kama mwalimu bomba ambaye hakuwa na mazoea ya kuingia darasani na vitabu kama walimu wengine, bali angefunza zaidi ya masaa mawili kutoka kichwani mwake tu. Mgeni Rasmi alisema hakuna Kiswahili kibovu, bali kuna viswahili vingi tu, kwa hivyo hatufai kuonea aibu Kiswahili tunachokizungumza. Alimtaja Ken Walibora kama mwandishi aliyekuwa na mshawasha wa kutoa vitabu vingi vilivyotokana na maisha ya kawaida ya binadamu. “Niliwahi kumpigia simu na kumsifia ya kuwa akiendelea kuandika vitabu kama anavyoandika, atakuja kuwa mwandishi tajika siku moja”, alisema Prof. Senkoro. Mgeni Rasmi alisema kuwa anazienzi kazi za Ken Walibora kwani maandishi yake mengi yalimkumbusha maisha aliyoishi akiwa kijana mdogo kule kijijini. Alisema kazi za Ken Walibora zinafaa kutazamwa na kuchambuliwa kifalsafa kwa sababu maandishi yake yana mafunzo mengi mno. Ken Walibora alikuwa na malengo yake maalum ya kukiendeleza na kutukuza Kiswahili. Alimalizia hotuba yake kwa kusema, “huwi Muafrika kwa kuzaliwa ndani ya Afrika, bali unakuwa Muafrika kwa Afrika kuzaliwa ndani yako.” Kazi za Ken Walibora zimeeleza vizuri maana ya maisha, na kifo chake kimenyakulia familia ya Kiswahili rasilimali kubwa mno.

Prof. Inyani Simala alikisifu Chuo Kikuu cha Kibabii kwa kutenga muda na rasimali kumuenzi mtetezi wa lugha ya Kiswahili duniani. Aliwahizima wahudhuriaji kutilia maanani mada ya mhadhara wa kumuenzi Ken Walibora kwani sisi sote tuko safarini. Alimkumbuka Ken Walibora kama mtaalam aliyetumikia Jamii kwa kutumia lugha kama falsafa na chombo cha kuhamasisha Jamii. Prof. Simala alimsifu Ken kwa kuzienzi lugha zingine na kutotaka lugha tofauti tofauti kuwa na uhasama. Kazi za Ken za Kisanaa zilisisitiza swala la utambulisho la Waafrika na utamaduni wao, swala ambalo ni muhimu sana katika Taaluma ya Kiswahili.

Wengine waliohudhuria mhadhara huo ni wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu vya Moi, Egerton, Embu, Jaramogi Oginga Odinga na Masinde Muliro.